Je wajua nini kuhusu Kasa? (Sea Turtle)

Published on by Boniventure Mchomvu

Mtoto wa kasa Baada ya kutotolewa na kutoka kwenye shimo ambamo kasa mkubwa aliweka mayai yake

Mtoto wa kasa Baada ya kutotolewa na kutoka kwenye shimo ambamo kasa mkubwa aliweka mayai yake

JE WAJUA KUHUSU KASA KIUMBE WA BAHARINI MWENYE MAAJABU KATIKA MAISHA YAKE

Viumbe wengi baharini wapo katika hatari ya kutoweka duniani, hii ni kutokana na uharibifu wa mzalia na makazi ya viumbe hao. Kasa ni miongoni mwa viumbe wa baharini walio katika hatari ya kutoweka duniani kutokana na kupungua kwa idadi yao duniani kote. Kwa mara ya kwanza kasa wameonekana duniani miaka milioni 200 iliyopita. Kasa pia ni miongoni mwa viumbe wa baharini wanaotembea umbali mrefu katika kutafuta makazi na chakula. Kasa wanao uwezo wa kutembea zaidi ya kilomita 3,500 (sawa na kutoka Kisiwa cha Mafia, Tanzania hadi Mogadishu nchini Somalia) kutoka katika mazalia yao hadi kwenye makazi au malisho yao. Hii imethibitika kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2012 na shirika lisilo la kiserikali la Sea Sense huko Kisiwani Mafia, ambapo kasa aliyekuja kutaga aliwekewa kiwambo cha satellite ambacho kiliweza kutoa mwenendo mzima wa kasa huyo. Kasa wametajwa kati ya viumbe wa baharini walio katika hatari ya kutoweka dunia kutokana na madhara yanayowakabili kutokana na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi. Sea Sense inajishughulisha na utunzaji na uhifadhi wa viumbe wa bahari walio katika hatari ya kutoweka duniani. Ilianza shughuli zake huko Kisiwani mafia mnamo mwaka 2001. Kwa sasa inafanya kazi zake takribani wilaya sita katika ukanda wa bahari ya hindi hapa Tanzania. Kuna aina saba za kasa duniani, kwa Tanzania kuna aina tano tu za kasa wanaopatikana ambao ni; Kasa Kawaida, Ng’amba, Duvi, Kigome na Kasa Noa. Aina mbili za kasa hazionekani katika bahari ya hindi na hii ni kutokana na hali ya joto la bahari ya hindi ili hali aina hizo mbili zinapendelea kuishi kwenye baharini zenye baridi. Kati ya aina tano za kasa zinazopatikana hapa Tanzania ni aina mbili tu zinazotaga katika fukwe za pwani ya ya Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania, aina hizo ni Kasa Kawaida na Kasa Ng’amba. Aina nyingine tatu zilizobaki zinatumia bahari ya hindi kama sehemu ya malisho na makazi tu, na hurudi katika nchi walizozaliwa kwa ajili ya kuzaliana na kisha kurejea tena katika malisho na makazi yao hapa Tanzania. Kwa kawaida kasa dume maisha yake yote huwa baharini, ila kwa kasa jike anatumia muda wake wa kutaga kutoka ndani ya bahari na kuja ufukweni kutaga mayai yake. Kasa wanataga katika fukwe zenye mchanga, ambapo hutoka baharini kwa kutambaa hadi ufukweni. Hapo huchimba shimo kwa ajili ya kuweka mayai yake. Kasa anatumia takribani masaa matatu hadi manne kwa ajili ya kuchimba shimo, kutaga, kufukia mayai na kisha kurudi baharini. Kasa ana tabia ya kutaga sehemu aliyozaliwa, hata kama atakuwa umbali gani, ikifika kipindi chake cha kutaga atarudi na kutaga katika fukwe aliyozaliwa. Kutoka kuzaliwa kwake hadi kuanza kutaga tena inachukua takribani miaka thelathini. Kwa maana hiyo ni kwamba hata kama malisho yake yapo nchini Somalia, ifikapo kipindi cha kutaga kasa huyu atarudi kutaga Kisiwani mafia katika eneo alilozaliwa miaka thelathini iliyopita. Kasa anataga mayai hadi 7000 katika maisha yake, hutaga mayai 80 hadi 180 kwa kiota na hutaga viota 4 hadi 6 kwa msimu ambapo kila kiota hupishana kwa wastani wa siku 10 hadi 14. Mayai ya kasa yanakaa aridhini kwa wastani wa siku 55 kabla ya kutotolewa. Msimu wote wa kutaga kasa anakuwa hali chakula hadi msimu uishe kwani tumbo linakuwa limejaa mayai, Baada ya msimu wa kutaga jike hurudi katika malisho yake na hatotaga hadi baada ya miaka 2 hadi 3. Utafiti unaonyesha kuwa ni mtoto mmoja tu kati ya 1,000 ambaye hukua nakufikia umri wa kutaga, na hii hutokana na athari za asili au zitokanzo na shughuli binadamu. Wastani wa maisha ya kasa ni miaka 80 hadi 100.

JE WAJUA KAMA KASA HANA MALEZI YA MAYAI WALA WATOTO WAKE?

Kasa haatamii mayai yake bali huyafukia na kuyaacha mpaka hapo yatakapojitotoa yenyewe, kwa kifupi ni kwamba kiumbe huyu hana malezi ya mayai wala watoto wake, akishakutaga basi kazi yake inakuwa imekwisha mayai yatajitotoa yenyewe na watotot wanatoka na kuelekea baharini kuanza maisha yao bila ya kumjua baba na mama yao.

KIASI CHA JOTO NA JINSIA YA WATOTO WA KASA…!!!

Kiasi cha joto la mchanga wa fukwe alipotagia kasa kina nafasi kubwa sana ya kupanga uwiano wa jinsia ya watoto watakao zaliwa katika kiota kile. Wastani wa joto linalotakiwa kwa uwiano sawa wa jinsia ya watoto wa kasa ni nyuzi joto 28. Kadri joto linavyozidi kupanda zaidi ya wastani huo asilimia kubwa ya watoto watakaozaliwa watakuwa majike na endapo joto litapungua katika wastani huo asilimia kubwa watazaliwa watoto madume. Pia wastani wa mayai kukaa chini ya mchanga inategemea na joto la mchanga, endapo joto litakuwa kubwa, wastani wa kukaa chini utakuwa chini ya siku 55 na kama joto litakuwa chini ya wastani, mayai yatakaa chini ya ardhi kwa zaidi ya siku 55 kabla ya kutotolewa. Tofauti na kipindi cha kupandana kasa hutumia muda wao mwingi kwa kula na kupumzika, kwa lugha nyepesi twaweza sema hawa ni viumbe ambao hawana muda wa kupiga umbea. Asilimia kubwa ya kasa hula viumbe wabahari kama jellyfish, sponges matumbawe, kaa, kamba na samaki, Kasa pekee anayekula majani ya baharini ni kasa kawaida kipindi anapokuwa mkubwa.

MADAHARA YANAYO WAKABILI VIUMBE HAWA ADIMU..!!!

Kasa anakabiliwa na madhara/matishio mengi ambayo mengi ni matokeo ya shughuli za binadamu. watu wanawinda kasa kwa ajili ya nyama yake na pia wapo wanaochukua mayai ya kasa kwa ajili kula na kuuza. Kasa wengi wameripotiwa kuuwawa kwa ajili ya nyama katika pwani ya Tanzania. Uvuvi haramu pia umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa katika kupungua kwa kasa hususani kwa Tanzania. Hii ni kutokana na kuharibiwa kwa makazi, malisho na mazalia ya kasa na viumbe wengine wa baharini walio katika hatari ya kutoweka duniani. Uchafuzi wa mazingira pia umekuwa ni moja kati ya athari zinaowakabili viumbe hawa hususani pale makazi na malisho ya yanapokuwa yamechafuliwa na kupelea wao kula plastic wakidhani ni jelly fish ambacho ni chakula chao.

JE! SHERIA INASEMAJE KUHUS VIUMBE HAWA ADIMU…!!!

Sheria na kanuni ya uvuvi ya Tanzania inasema wazi kuhusu hawa viumbe. Kwamba hairuhusiwa kwa mtu yeyote kuharibu mazalia, malisho na makazi ya viumbe hawa adimu walio katika hatari ya kutoweka duniani. Pia sheria na kanuni zimeainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote kumiliki au kusababisha mtu kuwa au kumiliki zao lolote litokanalo na viumbe wa bahari walio katika hatari ya kutoweka duniani akiwemo kasa. Kanuni ya uvuvi ya Tanzania bara namba 67 (i hadi iv) ya mwaka 2009 inafafanua na kuelekeza ulindaji na utunzaji wa viumbe hawa.

JE! KASA ANAUMUHIMU GANI…?

Kasa wanaumuhimu sana katika mustakabali mzima wa ikolojia ya bahari na pwani kwani; kasa husaidia kupunguza virutubisho vya baharini na nchi kavu, husaidia katika mzunguko wa chakula baharini (Food web and chain), ni muhimu katika kutambua uhai na maisha ya pwani na mazingira yake, wana umuhimu katika tamaduni na mila za watu wa pwani, hutumika katika utafiti na utoaji wa elimu na pia ni chanzo cha ajira na mali asili ya kukumbukwa (Utalii).

Kasa jike akiwa anataga katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Kasa jike akiwa anataga katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Watoto wa kasa wakitoka kwenye kiota chao tayari kuelekea baharini kuanza maisha yao katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Watoto wa kasa wakitoka kwenye kiota chao tayari kuelekea baharini kuanza maisha yao katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Kasa akirejea baharini baada ya kumaliza kutaga katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Kasa akirejea baharini baada ya kumaliza kutaga katika fukwe mojawapo hapa Tanzania

Published on Conservation

To be informed of the latest articles, subscribe:
Comment on this post